News
Training
Uhifadhi na Matumizi Sahihi ya Misitu, Mito, Mabwawa na vyanzo vya maji.
April 14, 2026
By Rashid Ligaya
Mafunzo ya uhifadhi na matumizi sahihi ya misitu, mito, mabwawa na vyanzo vya maji.
Mradi wa FOLUR kwa kushirikiana na wadau wa mazingira (SUMMA) pamoja na wataalamu wa Kitengo cha Maliasili na Mazingira kutoka Halmashauri ya Wilaya Mlimba wametoa mafunzo kwa wajumbe 12 wa Kamati ya Maliasili na Mazingira katika Kijiji cha Merera, Kata ya Chita. Mafunzo haya yamelenga kuwajengea uwezo wajumbe wa VNRC’s pamoja na viongozi wa kijiji ikiwemo Mtendaji wa Kijiji (VEO) katika usimamizi endelevu wa rasilimali za asili. Washiriki wamepata uelewa wa kina kuhusu uhifadhi na matumizi sahihi ya misitu, mito, mabwawa na vyanzo vya maji. Aidha, mafunzo haya yameweka mkazo katika uwajibikaji na ushirikiano kati ya jamii na taasisi za mazingira. Uchaguzi wa wajumbe umezingatia usawa wa kijinsia pamoja na uwakilishi kutoka kila kitongoji.
Kupitia mafunzo haya, wajumbe wamewezeshwa mbinu bora za kulinda na kusimamia rasilimali za kijiji kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo. Viongozi wa kijiji wamehimizwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa sheria ndogo za mazingira na kushirikisha wananchi katika shughuli za uhifadhi. Mafunzo haya pia yamelenga kuongeza ufanisi wa kamati katika kufanya maamuzi sahihi yanayohusu maliasili. Jamii imeaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda mazingira ili kukabiliana na changamoto za uharibifu wa rasilimali. Hatua hii inatarajiwa kuleta mabadiliko chanya katika usimamizi wa maliasili Kijiji cha Merera.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Mlimba, Ndg. Jamary Idrisa Abdul, amepongeza na kuunga mkono juhudi za utunzaji wa maliasili na mazingira zinazofanywa kupitia mafunzo hayo.
Amesisitiza umuhimu wa kuendeleza usimamizi endelevu wa rasilimali kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Aidha, amewahimiza wajumbe na viongozi wa vijiji kutumia elimu waliyoipata kulinda mazingira yao.
Ameeleza kuwa Halmashauri itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuimarisha uhifadhi wa maliasili.