MIFUMO YA KIDIJITI KULETA MAPINDUZI YA KILIMO NA MAZINGIRA MRADI WA FOLUR
News Training

MIFUMO YA KIDIJITI KULETA MAPINDUZI YA KILIMO NA MAZINGIRA MRADI WA FOLUR

May 24, 2026 By Anangisye Mwateba

Watumishi wa mradi wa Mfumo wa Chakula, Matumizi ya Ardhi na Urejesho (FOLUR) kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wafundishwa namna ya kutumia mfumo wa kujaza taarifa mbalimbali za shughuli wanazozifanya


Watumishi wa mradi wa Mfumo wa Chakula, Matumizi ya Ardhi na Urejesho (FOLUR) kutoka Zanzibar na Tanzania Bara wamekutana katika Manispaa ya Tabora, kupata mafunzo ya namna bora ya kutumia mifumo ya kidijitali katika utendaji wao wa kila siku. Mratibu wa mradi huo, Bw. Wanjala Mgaywa, amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatasaidia watendaji kupanga na kusimamia matumizi ya ardhi kwa tija. Aliongeza kuwa matumizi sahihi ya mifumo hiyo yatawezesha upatikanaji wa takwimu sahihi zitakazowasaidia wakulima wadogo kuzalisha kwa wingi katika maeneo madogo bila kuharibu mazingira. Juhudi hizo pia zinachangia upunguzaji wa uzalishaji wa hewa ya kaboni, jambo ambalo litaleta manufaa makubwa ya kiuchumi kwa halmashauri husika na taifa kwa ujumla. Bw. Mgaywa alisema kuwa mafunzo hayo yanajenga uwezo wa wataalamu kutumia mifumo ya kisasa kufuatilia urejesho wa mifumo ya ikolojia, usimamizi wa ardhi, na utekelezaji wa mradi vijijini. Lengo lingine ni kuimarisha mifumo ya uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya bajeti ya mradi. Aidha, mratibu huyo alibainisha kuwa mafunzo hayo yanalenga kuoanisha utendaji kazi kati ya sekta za kilimo, ardhi, misitu, na mazingira, pamoja na kuweka mifumo thabiti ya kukusanya data ili kupima matokeo chanya kwa jamii. Mradi wa FOLUR unafadhiliwa na Mfuko wa Dunia wa Uhifadhi wa Mazingira (GEF) na kuratibiwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Zanzibar. Mradi huu una thamani ya takriban Shilingi bilioni 18.35 na unatekelezwa katika Halmashauri ya Mlimba mkoani Morogoro ukilenga kilimo endelevu cha mpunga na Halmashauri ya Kaskazini 'A' na Halmashauri ya Kaskazini B mkoa Kaskazini Unguja, ukilenga kukuza zao la Mpunga, karafuu, kakao, na urejesho wa misitu.
Back to News & Events
Details
Published Date:

May 24, 2026

Category:

News

Type:

Training