Event
Update
MAFUNZO JUMUISHI KWA WATAALAMU WA KONGANI YA ZANZIBAR
June 08, 2026
By Anangisye Mwateba
USIMAMIZI JUMUISHI WA RASILIMALI KULETA TIJA KATIKA MAENDELEO-KATIBU MKUU WIZARA YA KILIMO ZANZIBAR
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Bw. Salehe Mohamed Juma amewataka wataalamu kutoka katika Sekta za Ardhi, Maji, Kilimo, Misitu na Uhifadhi wa Mazingira ambao wanapatiwa mafunzo ya Usimamizi Jumuishi kuwa chanzo cha mabadiliko chanya yenye kuleta tija kwa jamii katika suala zima la usimamizi wa rasilimali za maliasili.
Akifungua mafunzo hayo yanayofanyika katika ukumbi wa ofisi za Wizara zilizopo Maruhubi Zanzibar, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa wataalamu hao wamepata fursa adhimu ya kujifunza mbinu bora za usimamizi jumuishi wa maliasili ili kutunza rasilimali muhimu za nchi.
“Kupitia mafunzo haya, tunatarajia kuona mabadiliko chanya katika usimamizi wa rasilimali zetu, ikiwa ni pamoja na matumizi sahihi ya ardhi, maji, kilimo, misitu, uhifadhi wa mazingira na kuongeza thamani rasilimali zetu ili kuinua maisha na kukuza uchumi katika mikoa yetu,” alisema Katibu Mkuu.
Mafunzo hayo yanatolewa na wakufunzi kutoka Taasisi ya Kutathimini Rasilimali (IRA) iliyo chini ya Chuo Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) na kufadhiliwa na Mradi wa Mifumo ya Chakula, Matumizi ya Ardhi na Urejesho wa Mandhari ya Misitu nchini Tanzania (FOLUR).
Akimkaribisha Katibu Mkuu, Mratibu wa Mradi wa FOLUR Bw.Wanjala Mgaywa alisema kuwa mradi uliona kuna ulazima wa kuwa na mafunzo ya namna bora ya usimamizi jumuishi wa rasilimali za maliasili ili kuweza kuyafikia vizuri malengo ya Mradi.
Aidha Bw. Wanjala aliongeza kuwa wataalamu kutoka IRA walipofanya utafiti wao kuhusu usimamizi wa rasilimali za maliasili waligundua kuwa taasisi zimekuwa zikisimamia sekta zake kipekee hatua ambayo haileti tija, hivyo katika matokeo yao waliona uko umuhimu wa kuwa na usimamizi jumuishi wa rasilimali za maliasili ili kuleta tija kwenye jamii.